Mchanganuo wangu wa Kitabu: Nyalandu F., UNAWEZA: Mbinu Kumi Za Kumudu Masomo Yako (Dar-es-Salaam: Shule Direct, 2014), pp. 56

Wakati ambapo Tanzania imekumbwa na janga la elimu mbovu na hivyo mijadala mbali mbali kuhusu elimu na namna ya kuiboresha, kuna ambao wamebaki kuongea na kulalamika lakini kuna waliochukua hatua. Kati ya waliochukua hatua madhubuti ya kupambana na janga la elimu mbovu Tanzania ni Faraja Nyalandu. Kwa hapa sitaongelea mengi aliyoyafanya katika hili lakini nitachambua, kwa unyenyekevu, kitabu alichoandika kiitwacho : Unaweza: Mbinu Kumi za Kumudu Masomo Yako.

Kitabu kinaeleza kwa lugha nyepesi namna 10 za kujifunza na kumudu masomo. Namna hizi ni (1) Kutambua Kwa  Nini Uko Shuleni; (2) Fahamu Lugha inayotumika kufundishia; (3) Elewa Somo; (4) Zingatia Matumizi ya Muda Wako; (5) Jifunze Kutafakari; (6) Jifunze Ulichojifunza; (7) Kuwa na mkakati binafsi;(8) Ushirikiano; (9) Kuwa na Uvipendavyo nje ya masomo; na (10) Mwamini Mungu.

 Kwa makini sana Faraja anaelezea kila mbinu, anaonyesha umuhimu wa kila mbinu na pia anaonyesha jinsi ambavyo hizi mbinu zinategemeana. Hivyo ni muhimu kwa mwanafunzi kuelewa mbinu zote hizi ili aweze kumudu masomo yake.

 Muhimu zaidi ni jinsi Faraja anavyounganisha uelewa wa masomo darasani na maisha ya kila siku. Elimu inatusaidia katika utatuzi wa matatizo ambayo tunakutana nao kila siku maishani. Hivyo anaonyesha uelewa ni muhimu kuliko kukariri.  Zaidi pia anaunganisha uelewa na maisha kwa kuonyesha umuhimu wa ushirikiano na pia kuwa na muda na mambo mengine nje ya masomo. Mambo yote haya ni muhimu.

 Kwa muda sasa kumekuwa na mjadala kuhusu lugha ya kufundishia hapa Tanzania hususan matumizi ya lugha ya kingereza kwenye shule za sekondari. Bila kuingia kwenye huyo mjadala Faraja anaonyesha jinsi lugha inaweza kufanya mwanafunzi asielewe na anatoa mfano wa wimbo wa Taifa ulioandikwa kwa kanji (Kichina). Ingawa watanzania wanaujua wimbo wa Taifa, kama umeandikwa kichina hatutautambua. Hivyo anaonyesha tu ni lazima kila mwanafunzi afanye bidii kuelewa lugha ya kufundisha ili aweze kumudu masomo. Anasema mwaka wa kwanza ni muhimu sana wanafunzi waelewe lugha ya kingereza na kanuni zake ili aweze kumudu masomo yake. Hili la lugha ni tatizo kubwa nchini na lazima Taifa (sisi wote) tuzidi kulifikiria ili kuleta suluhisho la maendeleo.

 Kwa hekima kubwa, Faraja ameonyesha mbinu ya mwisho ni kumwamini Mungu. Hili ni jambo la juu sana na kila mwanafunzi anayemwamini Mungu anafanikiwa kwa sababu hakubali vitisho au wasiwasi kumrudisha nyuma. Ndio sababu naona kitabu kinaitwa UNAWEZA, hili ni neno la kiimani na ni kweli kila mwanafunzi anaweza.

 Kitabu kimetumia rangi mbalimbali katika kurasa zake na pia michoro. Hii ni muhimu sana kwa kuvutia wanafunzi kusoma na pia kwa uwelewa rahisi. Kila mbinu imewakilishwa kwa rangi tofauti.

 Nilipata shida  kidogo nilipokuwa nasoma hiki kitabu haswa kwa kuona labda Faraja alifikiria zaidi wanafunzi walioko mijini au wenye uwezo flani. Maana Faraja alitoa mfano wa kupoteza muda kwenye mitandao. Nikajiuliza ni wanafunzi wangapi wana mitandao Tanzania? Lakini nilifurahishwa badae niliposoma mbinu ya “mkakati binafsi” niliona kati ya hatari ambazo Faraja alitaja zinazowekumkumba mwanafunzi  ni kama “kazi nyingi nyumbani.” Hapo wasiwasi wangu ulipungua nikajua mwandishi alifikiria pia wale wanafunzi wenye uwezo duni wa kimaisha ambao wanakumbwa na hatari kama hizi.

 Naona pia Faraja angeongelea zaidi au kuweka mkazo zaidi juu ya “kutambua vipawa”. Ingawa Faraja aliongea hili kwa mbali na kutoa mfano wa maisha yake na uandishi (alivyokuwa akitengeneza kadi na kuandika maneno mazuri akiwa mwanafunzi) angeweza zaidi kuongelea jinsi ya kutambua vipawa na kuvikuza. Hili simlaumu, na labda iwe changamoto yetu wengine sisi kuliandikia.

 Binafsi ingawa nimesoma na kumudu masomo mpaka shahada ya uzamivu (PhD) nimejifunza mambo mengi sana  kwenye hiki kitabu. Nimejifunza umuhimu wa kutafakari na kujifunza nilichojifunza. Niliwahi kufundisha kwa miaka 3 katika chuo kikuu cha Nottingham, na kama mwalimu ilinibidi nisome na kujitayarisha sana ili niweze kufundisha vizuri. Nafikiri baada ya kuacha kufundisha nilisahau kidogo kiwango cha elimu nilichokuwa napata kwa kujitayarisha na somo. Lakini kitabu hiki cha UNAWEZA kimenikumbusha na kunionyesha kuwa, hata kama sifundishi, ninaweza bado kujifunza ninacho jifunza.

 Asante sana Faraja kwa kitabu kizuri. Asante kwa kuchukua hatua katika mapigano ya kuboresha elimu Tanzania. Nawasihi wazazi wanunulie watoto wao hiki kitabu na wasome nao. Kama unauwezo nunulia pia watoto wengine kwenye shule mbali mbali.

One thought on “Mchanganuo wangu wa Kitabu: Nyalandu F., UNAWEZA: Mbinu Kumi Za Kumudu Masomo Yako (Dar-es-Salaam: Shule Direct, 2014), pp. 56

Leave a Reply

Your email address will not be published.