Kuhusu Kura Ya Wazi au Kura Ya Siri #BungeKatiba

Baada ya msuguano wa #Posho, Bunge letu maalum la Katiba limepoteza karibu wiki nyingine nzima kubishana kuhusu uamuzi wa kuwa na Kura ya Wazi au Kura ya Siri.  Tayari wiki mbili zimepita la Bunge la siku 70 (wiki 7) lakini yaliofanyika ni majadiliano ya Posho na hili la kura.

Hili linatuonyesha kabisa wengi wa wakilishi wetu katika hili Bunge wameenda zaidi kimaslahi yao binafsi au ya kichama. Tunachosahau ni kwamba hili ni Bunge maalum la Katiba na walionda huko ni wawakilishi wa wananchi na maslahi yanatakiwa yawe ya wananchi na nchi yetu kwa ujumla (national interests).

Ingawa nimejitahidi sana kunyamaza huku nikifatilia mitandaoni na kwenye magazeti, nimeona nisiendelee kunyamaza. Wiki hii nilichambua kitabu cha Chinua Achebe  ‘There Was A Country: A Personal History of Biafra’ na kati ya mambo ambayo Achebe alihimiza ni kuwa waandishi lazima washiriki katika harakati za kisiasa. Kwa maneno mengine lazima waandike la sivyo watakuwa tu kama “footnotes”. Hilo ndo nililojifunza sana na ukisoma uchambuzi wangu utaona ata nimenukuu aya nzima kutoka kwa Achebe kuonyesha umuhimu wa kuandika. Hivyo nami nimeona nisikae kimya tena kuhusu hili swala la Kura ya Siri au Kura ya Wazi.

Kidemokrasia kabisa na kwa mantiki ya Bunge Maalum kama hili la Katiba hoja yenye nguvu ni ya Kura Ya Wazi. Kwa nini?  Kwa sababu zifuatazo:

  • Bunge hili linawakilisha wananchi katika makundi mbali mbali. Waliotumwa ni wawakilishi wa hayo makundi hivyo wanatakiwa maamuzi yao yawe wazi ili wanaowakilishwa wajue wawakilishi wao walisimamia lipi.
  • Kusema kuwa wawakilishi wataogopa vyama vyao na hawatakuwa na uhuru wa kusimamia wanachoamini ni UOGA na pia KUZALALISHA utume ambao wawakilishi hawa wamepewa na makundi yao na pia Rais. Wewe kama umepewa utume na nafasi kama hii ni kwamba umeaminika kuwa una uwezo wa kuchambua na kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya wananchi na Taifa. Kwa nini uogope leo kusema kwa wazi msimamo wako?
  • Kura Ya Wazi itasaidia wajumbe KUWAJIBIKA na maaumuzi waliofanya.  Nimekumbuka sana kampeni za 2008 za Marekani ambapo Obama alimshinikiza Mama Clinton kuwajibika na kura yake ya kupitisha vita vya Iraki.  Kura za jambo lile muhimu zilikuwa za wazi na ndio maana inajulika ni nani alipigia nini. Uingereza wabunge nao wanapiga kura za wazi kwenye mambo muhimu na wale ambao wanapingana na misimamo ya vyama vyao wanajulikana na huwa wanaitwa “rebels”. Na hii ni ilama ya demokrasia maana mtu ana uhuru wa mawazo na msimamo wake.  Kwa mifano zaidi na michanganuo juu ya “rebellions in parliament” angalia http://revolts.co.uk/?p=711 . Kwa hiyo hakutakuwa na neno kukiwa kuna “rebels” ambao watapingana na misimamo ya vyama vyao katika vifungu flani flani vya katiba. Huu ndio utashi wa kidemokrasia. Mbona Mbunge Esther ameweza kuwa kinyume na msimamo wa chama chake na kutetea kura ya siri? Hivyo angeweza pia kupiga kura ya wazi kwa jambo ambalo si sawa na msimamo wa chama chake.

 Kwa kusema haya si kwamba nafungia macho hoja za wanaotetea Kura ya Siri. Hapana. Hawa wana hoja lakini hoja yao sio ya kidemokrasia, ni ya ki “context”. Kwa maana wanajua kuwa wajumbe wengi ambao ni wa CCM wataogopa kuwa na msimamo tofauti ya chama chao kama watapiga kura ya wazi.

Hoja nyingine ya kura ya siri ni “mazoea”. Nimesikia wengi wakitoa mifano ya kura zinapigwa kwa siri, lakini hili ni Bunge la Katiba na kura zitakazopigwa sio za “kumchagua mtu” ni za vifungu vya katiba. Kwa nini iwe siri?  Ingekuwa ni kura za kumchagua mgombea wa nafasi flani sawa, lakini ni ya kupitisha kifungu cha katiba kwa niaba ya wananchi. Hivyo hamna haja ya siri.  Kura za siri zitafanyika wakati wa referendum ambapo kila mwananchi, binafsi kama mwananchi, ataamua uamuzi wake. Hapo Bungeni mko kama wawakilishi kwa maslahi ya makundi mnayo yawakilisha na wanananchi kwa ujumla na sio kwa maslahi yenu binafsi.

 Kwa ufupi ninasema, kama wewe ni mjumbe na hauwezi kusimamia unachooamini na kukisema wazi…huna maana maana hutaki kuwajibika. Tanzania tuacheni uoga.

8 thoughts on “Kuhusu Kura Ya Wazi au Kura Ya Siri #BungeKatiba

  1. Anonymous

    Huu mjadala ni wamoto sana. Unaposema kura za wazi ilituje tuwahujumu huko mbeleni sio sahihi…hatupo hapa kuhukumiana, wala hatujui kama hii katiba kama itatupa hata fursa yamabadiliko yatayowezesha kuhukumu wasiowazalendo…sio muda wa ku experiment….

    Na support kura ya siri kwasababu ya mambo nilioyashuhudia kwenye bunge kwa miaka kadhaa iliopita…wabunge wa CCM wamepinga vipengele vya budget ,wanaitwa kwenyevikao… lakini wakirudi wanapitisha budget bila mabadiliko yoyote …na hakuna mwananchi au kundi lolote lililoweza kuwadhiti au kuwaadhibu wabunge wasiowazalendo..wabunge wameonyesha dhahiri wapo upande wa chama zaidi ya wananchi…either kwa kukosa uzalendo au uoga…..hatutaki ijirudie kwenye bunge la katiba…

    Tulishudia budget chafu ya wizara ya nishati na madini ilivyoptishwa… KATIBU MKUU JAIRI, alichangisha 50m kutoka kila shirika chini ya wizara yake iliwawape wabunge wapitishe budget….ingekua kura ya siri wabubge wazalendo wangepokea pesa (wasionekanr wasaliti wa chama na kuadhihiwa) na bado wakawa wazalendo na kuikataa budget

    Reply
    1. Anthony Uhembe

      Hapana kwa kura ya wazi hasa kwa hao wabunge wetu wa Tanzania. Tumesha jifunge mengi sana katika bunge la Jamuhuri na tumeona jinsi ushabiki ulivyo kwa kugonga meza tena wengine wakitokea usingizini. Na haiwezekani kufanya majaribio kwenye jambo nyeti kama hilo au hata kuwianisha na yale yanayotokea kwenye mabunge ya western. Kwa kuwa wengi wa wabunge wetu huwa wanakuwa bendera fuata upepo au wa kukopi na kupesti, kisa jilani kanyoosha mkpno basi naye afanye hivyo. Kwenye hilp bunge la katiba wajumbe wasimamie kile wanachoamini kama wawakilishi wa wananchi na kuweka mbele uzalendo wao. Chaguo bura ni kura ya siri. Hatutaki majaribio hapa

      Reply
  2. OMBENI IKOLA

    UKWELI NI KWAMBA WABUNGE WATANZANIA HASA WA CCM KUSIMAMIA UKWELI BADO KABISA WAPEWE KURA ZA KIFICHO WANAOGOPA KUFUKUZWA

    Reply
  3. Anonymous

    Mimi nachowataka Wabunge wa Bunge la katiba waangalie ni kura ipi itafaa kwa Masilahi ya Taifa na si kwa masilahi ya chama au kiongozi binafsi

    Reply
  4. chacha heche

    kura maana yake ni maamuzi binafsi yasiyohitaji influence ya mtu flani
    lazima tukubaliane na ukweli kuliko marembesho yanayoandaliwa CCM walishaandaa mkakati wao kichama na wakatoka na msimamo wanataka kutumia bunge kupima nani hasa anayepingana na misimamo yao kwa maslahi yao hili ni hapana

    Reply
  5. chacha heche

    so ndugu yaangu kura ipigwe ya siri na kama ni kura za wazi basi liwe ndio staili ya upigaji kura wa kitanzania

    Reply
  6. anony

    Kura iwe ya wazi bungeni. Wabunge ambao ni wajumbe wa bunge la katiba wako mule kama wawakilishi wetu sisi wananchi. Kwa mantiki hiyo kupiga kura ya siri ni kuwanyima haki ya wao kujua mwakilishi wao ameamuaje. Pili, wajumbe wengine wako kwa niaba ya makundi yao. Tusinyime hayo makundi kujua wawakilishi wao wamepiga kura kwa maslahi ya nani.

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published.